07/06/2026
TIMU YA MAFUNZO YA MATUMIZI SAHIHI YA VIUATILIFU YAWAFIKIA MAAFISA UGANI NEWALA VIJIJINI
Zoezi la utoaji mafunzo kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao la korosho limeendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala Vijijini, mkoani Mtwara, likiwahusisha maafisa ugani kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa kilimo wa korosho wa mwaka 2026/27.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mtafiti kutoka TARI, Stanslaus Lilai, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha maafisa ugani kutambua kwa usahihi dalili za magonjwa yanayoshambulia mikorosho pamoja na matumizi sahihi ya viuatilifu katika kuyadhibiti.
Alitaja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni Ubwili Unga na Braiti, ambayo yanaweza kusababisha upotevu mkubwa wa mazao endapo hayatadhibitiwa kwa wakati na kwa njia stahiki.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Bodi ya Korosho Tanzania, Shinje Ngalula, alisema Serikali inaendelea kutoa pembejeo za kilimo kwa mfumo wa ruzuku sambamba na elimu kwa wakulima na maafisa ugani, kwa lengo la kuongeza tija na kufikia malengo ya kuzalisha zaidi ya tani 700,000 za korosho katika msimu wa mwaka 2026/27.
Nao maafisa ugani walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata itawasaidia kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi, hasa katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kabla na wakati wa msimu wa uzalishaji.
Hata hivyo, wamebainisha kuwa baadhi ya wakulima bado wanakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na kutotenga bajeti ya kutosha ya maandalizi ya msimu mpya mara baada ya mavuno, jambo linalowafanya kushindwa kumudu baadhi ya gharama za uzalishaji licha ya uwepo wa pembejeo zinazotolewa kwa ruzuku.
Kwa mujibu wa maafisa hao, hali hiyo imekuwa ikiwakwamisha baadhi ya wakulima kuanza mapema shughuli za kilimo na kuwekeza kwa kiwango kinachohitajika ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao la korosho.