26/08/2026
Askari wa Jeshi la Polisi, wawili wamefariki dunia baada ya gari kuwagonga watembea kwa miguu katika eneo la Maili Moja, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, ajali hiyo ilitokea Agosti 25, 2026, majira ya saa 1:40 usiku katika barabara kuu ya Dar es SalaamโMorogoro, eneo la kivuko cha waenda kwa miguu.
Taarifa ya Polisi iliyotolewa leo, Agosti 26, 2026, imeeleza kuwa gari aina ya Toyota Noah, lenye namba za usajili T.804 ERM, lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mlandizi likiendeshwa na Josia Isaya Arute, mwenye umri wa miaka 34, mkazi wa Mlandizi.
Inadaiwa kuwa gari hilo lilipofika katika eneo la zebra, dereva alilipita kundi la magari yaliyokuwa yamesimama ili kutoa nafasi kwa watembea kwa miguu kuvuka barabara, kisha kuwagonga.
Katika ajali hiyo, askari wa Polisi, Izdory George Michael, alifariki dunia, huku askari mwenzake, Rehema Juma Magawa, akijeruhiwa kichwani na kukimbizwa katika Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, Rehema Juma Magawa alifariki dunia asubuhi ya Agosti 26, 2026, wakati akiendelea na matibabu.
Jeshi la Polisi limesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, ikisubiri taratibu za kusafirishwa kwenda makwao kwa ajili ya mazishi.
Baada ya ajali hiyo, dereva wa gari hilo alikimbia eneo la tukio. Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliendesha msako na baadaye kulikamata gari hilo katika eneo la Kwa Mfipa, Wilaya ya Kibaha, majira ya saa 8:40 usiku, likiwa limefichwa.
Gari hilo limepelekwa katika Kituo cha Polisi Kibaha kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na alama za barabarani, likisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.