05/20/2026
Rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa serikali yake imefanikiwa kujenga jumla ya nyumba 273,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, k**a sehemu ya mpango mkubwa wa makazi nafuu nchini humo.
Akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa mijini uliofanyika Baku, Azerbaijan, Ruto alisema tayari familia 8,000 zimekabidhiwa funguo za nyumba mpya, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kupunguza uhaba wa makazi mijini.
Ruto alieleza kuwa mpango wa nyumba nafuu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya serikali yake, inayolenga kuhakikisha wananchi wengi wanapata makazi bora na salama kwa bei nafuu.
Aidha, Rais huyo alisisitiza kuwa haki ya makazi ni ya msingi na inalindwa chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu, hususan Universal Declaration of Human Rights, ambao unaweka wazi kuwa kila mtu ana haki ya kupata makazi yanayostahili maisha ya utu.
Kauli hiyo imekuja wakati Kenya ikiendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya makazi katika miji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini na kati.
Serikali ya Kenya inasema mpango huo pia umechangia kuongeza ajira kwa vijana na kukuza sekta ya ujenzi kupitia ushirikiano na sekta binafsi.