05/12/2016
SEHEMU YA PILI.
UWEPO WA HEKTA MILIONI 29.4 ZA UMWAGILIAJI UNATOA FURSA KWA MAENDELEO YA KILIMO HAI.
Asasi iliyoundwa kwa ajili ya kuendeleza harakati za kilimo hai (organic farming) nchini ya Tanzania Organic Agriculture Movedment (TOAM) ilifanya warsha ya siku moja kuhusu uendelezaji wa kilimo hicho kwenye ukumbi wa Hoteli ya Lamada mjini Dar es Salaam , kilichojiri.
MIONGONI mwa yaliyojitokeza katika warsha hiyo ni ukweli kwamba Tanzania k**a itacheza karata zake vizuri, inaweza kuvuna pesa nyingi za kigeni kutoka Ulaya, Marekani na Japan kutokana na bidhaa zake za kilimo hai kuwa na soko kubwa huko.
Watu wengi huko wanataka kula chakula salama kinachotokana na mazao yaliyokuzwa kwa njia ya asili. Japan kwa mfano, imegeuza mwelekeo wa kutaka mazao salama yanayotoka Afrika baada ya soko la India na nchi nyingine za eneo hilo la Asia kuvurunda.
Hata hivyo, ilielezwa katika warsha hiyo ya kuwa wakulima wengi nchini hawana elimu ya kutosha kuhusu kilimo hicho hivyo fursa hiyo ya kuvuna fedha za kigeni huwapita hivi hivi. Pia hawana mtaji wa kutosha wa kuwawezesha kujishughulisha na kilimo hai, jambo linalokwamisha Tanzania kuuza bidhaa nyingi katika masoko ya nje ya nchi hasa Ulaya, Marekani na Japan.
Lakini Kilimo hai ni kilimo cha aina gani hasa? Ni kile ambacho hakitumii mbolea na dawa za viwandani katika uzalishaji wa mazao. Mazao ya kilimo hicho ndiyo sasa yaliyopanda chati Ulaya na hata hapa nchini kwa kuuzwa kwa bei ya juu kulinganisha na mazao yanayozalishwa kwa kutumia mbolea za chumvichumvi na dawa za viwandani.
Sababu ya mazao hayo kupanda bei ni moja tu. Ni mazao salama kwa afya ya mtumiaji. Hayana madhara ya muda mfupi wala mrefu hivyo mtumiaji hahofu kupatwa na wakati wowote ugonjwa wa saratani na magonjwa mengine.
Utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa bei za mazao katika soko la dunia ambayo hayakutumia kemikali aina yoyote imekuwa ikiongezeka kulinganisha na yale ambayo yamekuwa yakitumia kemikali hizo. Wakati bei za mazao k**a kahawa, pamba na sukari zimekuwa zikiyumba katika soko hilo, bei za mboga mboga katika soko hilo imekuwa ikiongezeka na kuwapatia fedha nyingi wakulima wanaolima zao hilo kwa kutumia mfumo wa kilimo hai.
Lakini kwa mujibu wa washiriki kadhaa wa warsha hiyo waliozungumzia jambo hilo la mazao ya kilimo hai kuwa salama zaidi kiafya huwapumbaza wakulima wanaoelimishwa hivyo kwa mara ya kwanza.
Hujiuliza k**a mbolea za chumvichumvi za viwandani zimetokea Ulaya, na wamepata na wanaendelea kupata fedha nyingi kutokana na kuuza mbolea hiyo, ni vipi sasa, watu hao hao wa Ulaya hawapendelei kula vyakula vilivyokuzwa na mbolea yao na badala yake wapendelee vyakula vilivyokuzwa na mbolea ya asili?
Hata hivyo, wanaharakati wa kuendeleza kilimo hai huwa wanafanikiwa kuwashawishi wakulima kujihusisha na kilimo hai baada ya kuelezwa faida za kuuza kwa bei ya juu na umuhimu wa kutunza mazingira. Mkulima mmoja alisema ya kuwa unapoanza kujishughulisha na kilimo hai ambacho hakitumii kemikali unaona kuwa uzalishaji unakuwa mdogo lakini kwa kadri unavyoendelea uzalishaji unakuwa mkubwa.
Wale waliojikita katika kilimo hiki mwanzoni huweza kukiona kuwa hakina manufaa, lakini taratibu hujikuta wanafaidika maradufu hasa wanapolima mbogamboga, matunda na hata kufuga kuku ambao mayai hayawi na kemikali.
Taratibu kilimo hai sasa kinakuwa chaguo la wakulima wengi, kutokana na ukweli kwamba hakina gharama kubwa k**a inavyokuwa kwa kilimo cha kutegemea matumizi ya kemikali mbalimbali zinazotumika mashambani,wapo wakulima ambao wanajitahidi kuzingatia viwango vinavyotakiwa vya kilimo hai ili bidhaa zao zinaweza nchini na nje bila matatizo yoyote.
Chanzo: Raia Mwema
www.agroexchange.co