25/09/2025
KILIO CHA WAFANYABIASHARA NA MAFUNDI MABANGO JUU YA TOZO ZA MABANGO...
KWA:
*>Mafundi Mabango na Wafanyabiashara Wadogo...
Tunawaheshimu viongozi wetu na tunatambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi. Sisi ni wachangiaji muhimu wa pato la taifa kupitia kodi, leseni, na ushuru mbalimbali tunaolipa kwa uaminifu.
*Tunaandika waraka huu kwa uchungu mwingi, huku mioyo yetu ikiwa imejawa na majonzi na wasiwasi mkubwa. Kilio chetu kinatokana na utaratibu mpya wa kutoza gharama za juu na zisizo na tija kwa MABANGO ya utambulisho yanayowekwa ndani ya fremu za biashara zetu – sio mabango ya kibiashara kwenye barabara kuu, bali yale yanayoelekeza na kutambulisha tu biashara zetu!
Inayotuvunja Mgongo:
* Mzigo Mara Mbili (Double Taxation): Tayari tunalipa Kodi ya Mapato (TRA), Leseni za Biashara, Ushuru wa Bidhaa, na Ushuru wa Usafi. Mabango haya ni zana za msingi za utambulisho na sio bidhaa za anasa. Kuweka tozo nyingine juu yake ni sawa na kututaka tulipe kodi mara mbili kwa kitu kilekile – yaani uwepo wetu kibiashara.
* Kukata Tamaa na Kujiendesha "Kibubu": Wafanyabiashara wengi wanatoa mabango yao kwa kuhofia tozo hizi. Hili linasababisha biashara zao kujiendesha "kibubu" – hazitambuliki, hazielekezi, na mwisho wa siku wanapoteza wateja na kupunguza mauzo. Hii inakwenda kinyume na lengo la Serikali la kukuza biashara na ajira.
* Kupoteza Ajira kwa Mafundi Mabango: Sisi mafundi mabango tunategemea shughuli hii kuendesha maisha yetu na kulisha familia zetu. Tozo hizi za juu zinasababisha wafanyabiashara kuacha kutengeneza au kubadili mabango, na hivyo kunyonya ajira zetu na kutufanya tuingie kwenye lindi la umaskini. Tunapoteza wateja, tunapoteza kipato, na tunashindwa kutoa huduma za kijamii kwa familia zetu.
LETU KWA SERIKALI:
Tunaiomba Serikali yetu, kupitia mamlaka husika, kufanya mapitio ya haraka na kuchukua hatua zifuatazo:
* KUONDOA KABISA TOZO: Tunaomba iondolewe kabisa tozo ya mabango ya utambulisho wa biashara ambayo yako ndani ya fremu za biashara au karibu kabisa na eneo la biashara, kwani tayari tumelipia leseni na kodi nyingine zinazotambua uwepo wetu.