Ujamaa Online

Ujamaa Online Tunatoa Elimu ya Ujasiliamali, Masoko na Kukuza Mitaji kwa Vijana kufikia Malengo yao Kiuchumi na Kifedha.

SAFARI ISIYOSAHAULIKA.                              Sehemu ya V. Nilichukua pikipiki kwa safari nyingine kutoka Stendi M...
09/05/2017

SAFARI ISIYOSAHAULIKA.

Sehemu ya V.

Nilichukua pikipiki kwa safari nyingine kutoka Stendi Mpya hadi Mwandiga usiku ule! Tulitembea takribani dakika tano tu kulipofika mitaa ya Kahabwa ndipo historia yangu na dereva yule wa pikipiki aliyekuwa akijulikana k**a Mack zilipobadilika kabisa.
"Nini kile mbele bro!" aliniuliza Mack huku akipunguza mwendo kwa haraka sana.
Ndipo na mimi nikatazama mbele kwa makini... "Mungu wangu tumekufa!"

Sasa endelea......

*****
Gari kubwa lililokuwa limefunga barabara kwa juhudi kubwa zilizofanywa na matingo wa magari yaliyokuwa yamekwama pale zilizaa matunda kwa kulizamua na kufanya safari kurejea k**a kawaida. Mama Jane alikuwa ni mmoja wa abiria waliolala pale usiku wa jana yake kungojea basi lao liweze kupita. "Sijui Mathias jana walifika wao" aliwaza mama Jane baada ya kuanza tena safari yao. Ilikuwa saa nne asubuhi wakiwa wameanza kusafiri tena. Safari hii kidogo ilitia matimaini kwa sababu hali ya anga ilikuwa shwari kabisa. Saa saba mchana walifanikiwa kuwasili Kigoma na basi lao la Adventure na kushusha mzigo aliokuwa nao na kutafuta usafiri wa kuelekea nyumbani.

*****
Wote wawili Mathias na Mack walipoteza fahamu na hawakuwa tena katika ulimwengu huu. Safari yao ya pikipiki baada ya kufika maeneo yale hakuna awezaye kueleza nini kilitokea. Katikati ya umati mkubwa sana wa viumbe ambavyo haikuwa rahisi kuvitambua kwa haraka Mathias na Mack walikuwa katikati huku wakihema kwa mchoko wa mwendo wa kilometa nyingi walizotembea. Ilisikika tamko huyo mrudisheni kwa sauti iliyokuwa ya ngurumo kuu. Iliyovunjavunja miamba na kupeperusha matawi ya miti minene duniani. Mathias hakuwa tena na dereva wake alijiona pekee huku fahamu zake zikiwa kawaida lakini mwenye hofu iliyojaa mwili wake wote!
Hakujua yuko wapi na amefikaje anachokumbuka alikuwa kwenye pikipiki na alikuwa anaelekea nyumbani usiku ule! Umati ule wa viumbe vya ajabu na kutisha uliendelea kuongezeka zaidi na zaidi huku ikiashiria kufanyika kwa kikao kikubwa sana ambacho ajenda zake hakuzijua muda ule.
Mathias alijiwazisha huku akitetema mwili wote ukiwa umelowa jasho. Muda wote yanafanyika hayo Mathias hakujua ni mchana au usiku! Hakuhisi njaa, kiu, wala haja yoyote kiasi ambacho hakuelewa. Wakati huo fikra zake zikikuwa kawaida kabisa k**a mtu anayeona yote yaendeleayo ingawa akili ilianza kupoteza kumbukumbu muda baada ya muda. Kilichomshangaza zaidi na kumpa mawazo aliyotaman kujua...pale yupo wapi? ...na kwanini? Alikosa majibu.
Akafumba macho yake yaliyokuwa yamelowa kwa kutiririkiwa kwa jasho akapoteza fahamu!

Mukajaga!!.....Mukajaga!!..... Mukajaga!!.... Iyoooh!!.... Iyoooh!!.... Nyimbo ziliimbwa kwa sauti kuu iliyomfanya Mathias azinduke ghafla. Alistaajabu kuona umati ule wa viumbe kwa hesabu ya harakaharaka ni watu wote wa dunia hii mara kumi na tano wakutanike mahali pamoja yaani sehemu k**a ukumbi. Viumbe vile viliendelea kuimba na kucheza kwa kutikisa masingo ya vichwa vyao. Vilifurahi sana! Mathias alipepesa macho yake huku na huko kwa hofu na woga wa ajabu sana.
Viumbe vyote viliketi na kufanyiza hadhara kuu ambayo Mathias hakuwa na jeuri tena hofu, woga, wasiwasi vyote vililindima ndani ya mwili wake. Muda wote hayo yakitokea alikuwa amelala mahali ambapo muda wote alipigwa na vitu k**a mawimbi yaliyomfanya masikio yake kuanza kupoteza uwezo wa kusikia vizuri. Halikuwa amelala juu ya vitu vilivyokuwa lojolojo k**a maji.
Baada ya umati ule kuketi sauti ya ilisikika ikiamrisha Mathias abebwe apelekwe mbele kabisa. Viumbe takribani milioni hamsini vilinyanyuka na kumtwaa Mathias juujuu na kumsogeza mbele.

*****
Mama Jane aliwasiri nyumbani salama salimini na kulakiwa na mwanae wa pekee Jane.
"Waaaooh.... Mama yangu...!!" Jane alimkimbilia mama yake na kumkumbatia kwa nguvu. Alifurahi sana kufika salama kwa mama yake kutokana na misukosuko aliyokuwa akimueleza wakati wote wa safari yake.
"Hamjambo hapa!" mama Jane aliuza huku akivua sweta na kuagiza aletewe maji ya kunywa ya baridi. Jane aliingia ndani na kuleta maji kwa mama yake.
"Ebu nenda pale sokoni kwa Hassan uone k**a mzigo wangu umemalizika kushushwa maana nineacha wanashusha" alimuagiza Jane na bila hata kuongeza neno akaelekea sokoni kuuangalia mzigo wa mama yake.

Akiwa anakunywa maji mawazo ya Mathias yalimjia na kuamua ampigie simu ili kujua k**a na yeye jana alifika salama.
"Mteja unayempigia hapatikani kwa sasa. Tutamtaarifu kwa sms atakapokuwa hewani!"
"Atakuwa ameishiwa moto!" alijisemea na kunyanyuka akaingia ndani na kuelekea chumbani kwake akavua nguo zake za safari akajifunga kanga kifuani akatoka nje na akaingia bafuni kuoga walau kuondoa machovu ya safari ya siku mbili njiani.
Jane punde akarudi na kumkuta mama yake amemaliza tayari kuoga na kutenga chakula wale pamoja.
"Ulikuwa hujala tu? "
"Ndio nilikusubili ufike kwanza"
"Sawa! Leta apa nje tu"
Wakaanza kula huko wakiongea mawili matatu mama na mwana!
"Alafu mama kuna mkaka kapotea ghafla na alikuwa yupo safarini wametangaza msikitini Shia" Jane alimwambia mama yake.
"Amepotea? Alikuwa ametokea wapi? " "Walisema Kahama"
"Mmmh ni hatari!"
"Alikuwa anaitwa Mathias kijana mwenyewe! " aliongeza Jane.
Mama yake akashtuka ghafla... "Mathiasss???"
"Unamjua mama!"
"Mungu wangu! Atakuwa anepatwa na nini huyu. Nimempigia sasa ivi simu yake na haipatikani. Nilikuwa nae basi moja na tuliongea sana hadi tukapeana namba. Jana yeye walitangulia na basi jingine!"......
Mama Jane hakuendelea tena kula akachukua simu yake na kuipigia namba ya Mathias. Akajibiwa vilevile k**a awali. Akapumua kwa nguvu akaingia chumbani. Jane hakuelewa chochote!

*****
Mukajaga ni sehemu ambayo katika vitabu vingi vya masimulizi ya kutisha palisimuliwa na watu wengi sana. Kila hadithi yake iliposimuliwa kila mtu alijawa na hofu na wasiwasi nyakati za usiku wakati wa kulala. Kitu hasa kilichokuwa kunaogofya ni namna ya mahali hapo maisha yake yaliyo ya kutisha yaliyojaa mauaji mengi ya haraiki ya mamilioni kwa mamilioni ya watu wake. Hakukuwa na kitu kinachoitwa haki za raia. Hakukuwa na kitu kinachoitwa mahak**a ili haki itafutwe hapo. Kila kitu na amri ilitoka kwa 'Fute'. Huyu ndiye mungu wa mahali hapa.
Huabudiwa na kutukuzwa.
Yeye ndiye mwanzo na mwisho.
Akisema amesema.
Akikataa amekataa.
Hufanyi lolote bila yeye kujua.
Ole wako awe na hasi yoyote na wewe ndiyo unakuwa mwisho wako.... Kifo ndio haki pekee anayesitahili yeyote nchini hapa.

Picha na ramani ya nchi hii inamkanganyiko mkubwa, huwezi kuipata katika fikra za kibinadamu. Pande zote nne zipo na mipaka yote ipo lakini nchi zote jirani hazina majina yanayozitambulisha. Hazitamkiki. Hazifikiki na wala haziishiki.
Mukajaga ilikuwa ya pekee.
Ukifika umefika.
Ukitoka umekufa.
Na ukifa binadamu huomboleza kwa vilio na machozi ya majonzi ya kupoteza wapendwa wao! Hadithi hizi ndizo ziliwafanya wengi kusisimka na kupatwa na hisia kali za wasiwasi. Hakukuwa na historia ya mwanadamu yeyote kufika huko. Mtu pekee aliyefanikiwa kufika yasemekana alifika huko kabla hajazaliwa na alikuwa ni mtoto wa mzee mmoja maarufu miaka mingi sana hata kabla ya wakoloni wa Kijerumani. Mzee huyo alijulikana kwa jina ya Nziza na aliishi zaidi ya miaka mia, mitaa ambayo sasa inaitwa Kisitwe. Binti Ndiyu alikuwa mke wa saba wa mzee Nziza. Alikuwa ndiye mke wa mwisho katika orodha ya wake zake.
Yalikuwa ni majira ya mvua nyingi alipobeba ujauzito wake wa kwanza. Ujauzito uliendelea kukua na afya yake ilikuwa njema isiyo na shaka yoyote. Miezi tisa iliwadia na mabadiliko ya uchungu ikiwa ni dalili za kujifungua alipata. Kwa kuwa ulikuwa ni ujauzito wake wa kwanza ilibidi wake wenzake wamuangalie kwa huduma na maandalizi ya kujifungua.

Muda ya jioni wingu lilitanda likiashiria kunyesha kwa mvua muda wowote. Binti Ndiyu akiwa amejilaza chumbani kwenye nyumba yake alianza kujisikia uchungu sana. Tumbo la uchungu lilimkata na hakuona msaada mwingine zaidi ya kumwita mke mwenzake mama Shala ambaye walitazama nyumba. Muda huo huo mvua nayo ilianza kunyesha kwa kasi huku ikiambatana na radi na ngurumo za hapa na pale. Mama Shala aliwaita wake wenzake tayari kujiandaa na kumsaidia mwenzao ajifungue salama. Uchungu uliendelea! Uchungu ukashika kasi!
Binti wa watu akajitupa huku na kule!
Akajinyonga akajipindua weee.... Uchungu ukawa uchungu....
Binti akasukuma na kusukuma lakini wapi....
Siku ikapita hali ikapoa...
Ujauzito upo palepale.
Hakuna aliyeelewa kilichotokea.

Siku zikasonga.... Miezi kumi na mbili ikatimia. Ujauzito wa Binti Ndiyu anafanikiwa kujifungua mtoto wa kiume. Hakuna aliyeamini kuzaliwa kwa mtoto yule. Akapewa jina la kiha la Kahitila yaani aliyevuka muda. Kahitila akaendelea kukua na kukua. Akiwa na umri wa karibu miaka miwili Kahitila alipotea ghafla katika mazingira ambayo hakuna anayejua chochote kuhusu yeye mpaka leo! Hapo ndipo jina la Mukajaga ilipotajwa na mzee mmoja mashuhuri katika uganga na utabiri pale kijijini. Hakuendelea zaidi kulitaja jina hapo wala kutoa habari zake kwa hofu za matendo ya mahali penyewe. Watu walibaki na taharuki.
Huyo ndiye mtu aliyetajwa kuwa alienda na akarudi ingawa alienda hajazaliwa yaani kile kipindi cha kupitiliza kwa ujauzito wake na kuondoka kwa kupotea wakati ambao hajaanza kuongea hata sentensi!
Mathias alikuwa Mugajaga.... Iliyotajwa vizazi na vizazi kwa hadithi ileile iliyoogofya karne na karne.
Itaendelea.......

Maoni na ushauri.
Email : [email protected]
WhatApp 0757536278.

07/05/2017

NGUVU MKONONI.

Sehemu ya III.

Mipango yote ya safari ya kuondoka nyumbani ilikamilika baada ya kumaliza kazi za shamba ambazo zilikuwa zinamfanya baba yake amnyime ruhusa ya kutoka nyumbani. Alifanya matayarisho kidogo hasa ya fedha ili aweze kijikimu pindi atakapofika mjini. Aliuza mbuzi zake mbili na kuku takribani sita na kupata jumla ya laki mbili na hapo ukawa mwanzo wake wa safari ya kwenda mjini Kahama.

********

Tarehe 12 huwa ni siku ya kumbukumbu ya kubwa kwa miasha ya Ally. Siku hii huwa anaikumbuka tena zaidi ya siku yake ya kuzaliwa kwa utamaduni aliojijengea kwa miaka mingi sasa. Unaweza kujiuliza hii siku ina nini? Kwanini aipe kipaumbele hivi? Maswali haya unaweza kukosa majibu ila pindi usikiapo Ally akiwaambia wenzake utashangaa na unaweza hata usimuelewe kwa haraka. Haikuwa desturi ya watu kukumbuka matukio waliyoyaamua wenyewe! Haikuwa desturi ya watu kukumbuka vitu walivyofanya wenyewe! Tena katika mazingira ya kuwafanya wengine waione ni karaha kwao maana hawakuona mantiki yake. Kwa hiyo hakupata kuungwa mkono sana lakini kwake ulikuwa humwambii kitu, ulikuwa hupenyezi neno na wala ushauti wowote wa kumfanya eti aonekane k**a mshamba! Yeye alikuwa tayari kuonwa vyovyote watu wamuonavyo, alikuwa tayari kusemwa vyovyote watu watakavyoamua kusema! Lakini yeye aliamua kuwa upande aliouchagua kuwa. Kwa misimamo hii aliyokuwa nayo alijitengenezea sifa ambazo zolikuwa tofauti sana na vijana wengine!
Ilikuwa ni tarehe ambayo yeye alitoka nyumbani katika historia yake ya maisha kwani hakuwahi kutoka nje ya kwao zaidi ya kwenda shamba na mbugani miaka yote. Kwahiyo kwake ndio alikuwa k**a amezaliwa upya.

Kutoka Seeke kijiji ambacho Ally alizaliwa kufika Kahama mjini hapakuwa mbali sana. Ulikuwa ni umbali wa kilometa takribani kumi na mbili kufika. Ni mahali ambapo hata kwa miguu unaweza kwenda na kurudi. Ni mahali ambapo watu wake hawakuwa na shauku ya kwenda tena kwa kufanya makao k**a aliyokuwa nayo Ally. Vijana wengi wa vitongoji vyao walilidhika na maisha ya kijijini tofauti na yeye. Vijana wengi hawakuona sababu ya wao kuondoka kwao na kwenda mjini tena kufanya makao. Kwa hiyo yeyote aliyesikia mpango wake alimpinga na kumuona limbukeni tu na k**a mtu anayeanza kuchanganyikiwa. "Uko kuna wahuni na wavuta mabangi yeye akae tu apige jembe! " alisema Maige aliposikia habari zake. Bro, tulia mimi simaanishi huku napakimbia hapana ila nataka kubadili upepo kidogo ili nione sa ntabanana na mzee mpaka lini? " alieleza Ally.
"Naona unaanza kuchanganyikiwa hivi unamjua Nyanda, Mabula na... Mbona wote bado wapo kwao na hawana mawazo k**a yako? Na wanakuzidi sana tu na bado wapo kwao wanalima?" Maige alihoji.
"Sawa nawafahamu lakini hawawezi kunifanya nisifanye hiki nikifikiriacho kwa sasa! Mimi napapenda sana mjini ingawa sikuwahi kwenda na sipajui ndio itakuwa mara ya kwanza ila nikienda mimi naenda kutafuta kabisa kazi ya kufanya"
Maige alimuona Ally k**a mtu mwenye akili sana mwanzoni ila kwa maongezi ya habari hizi za kuhamia mjini alimuona na kumchukulia kuwa ni mtu wa ajabu na aliyechanganyikiwa kwa sasa. Yote haya alikutana nayo lakini hayakumfanya asitishe adhima yake ya kwenda mjini. Aliamini lazima akatafute maisha mjini. Hakuona sababu ya yeye kuendelea kuishi kwao. Akafunga safari akaaga nyumbani akaondoka ingawa mzee Bakari hakuwa na kipingamizi chochote safari hii, akampa kila lenye kheri mwanae. Ally akatoka.

Majira ya saa nne hivi Ally alifika Shunu maeneo ambayo panamchangamko wa watu, akaingia kwenye mgahawa mmoja uliokuwa umeandikwa "Mama Njenje Cafe" ili anywe chai kidogo.
"Karibu kaka!" sauti ya Pamela ilimkaribisha Ally mle mgahawani.
"Asante! " alijibu.
Nikuhudumie nini? " Pamela aliuliza.
"Niletee chapati tatu na chai! " Ally aliagiza.
'Kuna chai ya rangi na ya maziwa, nikuletee ipi?" Pamela alifafanua na kuuliza.
"Leta ya rangi tu!"
"Sawa kaka! "
Alisubiri chai kwa muda kidogo kisha akamuona Pamela anakuja na sahani ya chapati na chupa ya chai. Akamtengea kwenye meza aliyokuwa amekaa na kumimina chai kwenye kikombe. "Karibu chai"
"Asante" alianza kunywa. Mara punde kidogo kaita. Samahani dada mimi mgeni mitaa hii hivi hapa ndio Shunu? Aliuliza.
Ndio! Kwani umetokea wapi? "
Seeke!
Sasa mbona sio mbali na hapa jamani!
Nikweli lakini sikuwahi kufika maeneo haya tangu nizaliwe. Ndio mara ya kwanza! Ally aliongeza.
"Oooh! Sawa karibu!"
Asante"
Pamela aliachana na Ally akaenda kumsikiliza mteja aliyekuwa ameengia muda huo.
"Aaaah mume huyo! Umekuja na zawadi ya mkeo lakini!" Pamela alimchangamkia mtu aliyekuwa ameingia. Alikuwa ni Amily mzaliwa wa palepale Shunu anayejulikana sana kwa kila mtu kutokana na uchapakazi wake.
"Itoke wapi muda huu we nilitee chai na chapati zangu k**a kawaida mengine baadae!" alijitetea.
Alionekana kuwa amekaa huku akiwa na vumbi la pamba kwenye nguo alizokuwa amevaa muda huo ingawa palikuwa bado asubuhi mida ya saa tano tu.
"Ulilala night jana? " Pamela aliuliza huku akimmiminia chai mezani kwake.
Siunajua tena tusipofanya kazi nyie hamkai ndani" alisema Amily
Ha!ha!ha! mwanamke huduma babu wee! " unafikiri ulinitoa nyumbani nikupe tu? "
"Acha matusi wewe hudumia wateja mnawishe braza hapa amemaliza sio unaongeaongea k**a chiriku! " alisema Amily huku akimtizama Ally na kumsabahi.
"Braza niaje"
"Shwari tu vipi job"
"We acha haya makazi ya wahindi yatatuuaga mapema"
"Ni kawaida braza"
Ally aliingiziwa msamiati mipya kichwani na hakuweza kupata maana zake kwa haraka wakati huo alikuwa amemaliza kunywa chai tayari.
"Nimetumia shilingi ngapi dada?"
"Elfu moja mia mbili tu!" Pamela aliju na kumkaribia Ally, alipokea noti ya shilingi elfu mbili na kwenda kumchukulia chenji yake.
Ally aliwaza namna gani aanze ili kuulizia chumba mitaa ile ili masuala mengine yaendelee akiwa na uhakika wa mahali pa kuegesha mbavu zake hata k**a ni chini.
"Hivi braza wewe mitaa hii ni mwenyeji", alimuuliza Amily
"Hee huyo kuna mtu asiyemfahamu hapa Shunu!", alidakia Pamela na kumpa chenji yake.
"Kwani we umetokea wapi?" Amily amuuliza
"Seeke!, nimefika asubuhi hii nimekuja kutafuta kazi.". Ally alijibu.
"Umefikia wapi na unatafuta kazi gani maana wengine kalamu ni mikono yetu" aliongeza Amily.
"Yeyote tu mi nafanya kikubwa niishi tu. Nitapata wapi chumba mitaa hii?" "Vyumba vyenyewe vipo. Ongea na Amily kakangu maana hata mimi chumba ninachokaa alinitafutia yeye!" alisema Pamela.
"Baada ya kukutafutia hutaki ata nikutembelee" alitania Amily.
"Sitaki wapi kila siku nashinda hapa we nae hushikiki"
"Nitakutembelea siku moja usiku"
"Haa masuala ya usiku sitaki nakuwa nimejichokea zangu"
"Braza achana na huyu kasuku maneno hayaishi, vipi umefikia wapi muda huu" Ally aliulizwa.
"Hapa unaponiona ndio nimefik!" alijibu.
"Sasa ngoja nimalizie kunywa chai tufanye michakato usiwaze!".
Huyu ndiye Amily maarufu mitaa yote kwa jina maarufu la 'Yasoda'
Chochote unachotafuta na kuhitaji pita kwake utakipata muda huohuo. Sasa yupo na Ally kijana mpya machoni mwake na anahitaji chumba na namna gani anaweza kuanza maisha ya utafutaji mitaa ile asiyojulikana na yeyote!

Punde Yasoda alimaliza kunywa chai na akalipia na kutoka pamoja na Ally wakaenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwake. Walitembea mpaka mitaa ya jirani na Reny Bar mitaa aliyokuwa anakaa. Wakafika na kuingia ndani. Ilikuwa ni nyumba kubwa yenye vyumba kumi vyote vya wapangaji ndipo alipokuwa amepanga chumba chake kimoja na kufanya shughuli zake za mihangaiko akitokea hapo.
"Karibu braza pangoni kwangu!" Ukiwa mitaa hii watu wananijua kwa jina la Yasoda kwa jina hilo utanipata kwa haraka ila jina langu halisi ni Amily nmezaliwa hapahapa Shunu na sijawahi kutoka kwenda kwingine.
"Asante Yasoda mi anaitwa Ally Bakari kwenu ni Seeke nimekuja huku kutafuta maisha braza!"
"We usiwaze kikubwa nguvu kazi zenyewe zipo"
"Ulisema kazi gani unataka"
"Yoyote tu napiga sichagui"
"Unaweza kazi ya kubeba vitu vizito lakini"
"Mi napiga siunajua kijijini ndio kazi zetu kaka"
"Basi poa tutaona ngoja tufanye kwanza ustaarabu wa pango"
"Utakuwa umenisaidia sana"
Yasoda akavua suruali na kubaki kwenye kaptula kifua wazi akatoka akaenda bafuni kuoga walau kukata usingizi na machovu ya usiku kucha!
Ally alibaki mule chumbani na kupepesa macho yake huku na kule na kuona vitu vingi ambavyo alikuwa hajawahi kuviona vikiwa mle ndani. Vitu vilikuwa vimepangwa vizuri na kwa utaratibu maalumu. Palikuwa na kitanda na godoro kubwa, palikuwa na kabati la nguo, meza ya radio na tv chini palikuwa na kapeti ya nakshi ya pundamilia mlangoni na kwenye dirisha palipambwa na mapazia yenye rangi ya kahawia yote yalifanya muonekano wa chumba uwe wa kuvutia sana. Ally alitazama kwa makini sana huku mawazo yake yote yakiwa kwenye kupata chumba tu na hakujali ataanzia kulalia nini wakati huo. Vyote alivyoviona mle ndani alimeza tu mate na kukaa kimya k**a kifaulongo.
Punde tu Yasoda alimaliza kuoga, akajiandaa na kutoka na Ally wakaingia mtaani!
Itaendelea....

Comment & share

06/05/2017

SAFARI ISIYOSAHAULIKA.

Sehemu ya III
------------------------------------------------------------------------
Tulisimama Nyakitonto kwa usalama zaidi, hali ya anga haikuwa inaruhusu kabisa. Mvua kubwa ikaanguka, mvua ya mawe ikanyesha! Ikanyesha! Ilikuwa kubwa ajabu sikupata kuona hata siku moja katika maisha yangu. Lakini kadri ilivyokuwa inanyesha hali ya hewa nayo ikaanza kuwa angavu tena. Pakawa shwari baada ya masaa mawili hivi, dereva na konda wakajiridhisha tukaanza safari tena!

Sasa endelea!

******
Simu iliita, kabla sijaitoa mfukoni ikakata, "Nani huyu anabeep" nilijisemea kimoyomoyo. Kuiangalia 'missed call' kumbe Kingson mwenyewe, mwanangu mmoja wa kitambo sana ambaye huwa hanitafuti k**a hakuna updates mjini. Wengi walimzoea kwa jina la utani na lilijulikana sana, huyu ndiye bingwa wa route za mjini, ukimwita 'Staff' hujisikia na kujiona fahari kwani hakuna daladala ambayo alikuwa akilipa nauli. Alijuana na kila konda hata k**a konda huyo atakuwa ameanza kazi leo. Nilijaribu kumpigia mara kadhaa ili nimwambie nipo ndani ya 'Adventure' naenda lakini simu hazikutoka, mtandao ulikuwa chini sana nikaachana naye na kurudisha simu mfukoni.
"Yesu wangu!" Sauti ya mama mmoja jirani upande wa pili wa siti niliyokuwa nimekaa ilisikika baada ya basi kukanyaga dimbwi la maji na kumrukia ndani na kumlowanisha na kumchafua kwa maji yale yaliyojaa tope la balaa!, kwa sababu wakati huo kioo chake alikuwa amekifungua kuruhusu hewa iingie kidogo. Nilishtuka baada ya kuwa nawazo yalikuwa yameshafika mwisho wa safari.

Hali ilikuwa mbaya sana safari ilikuwa safari, kila abiria akaanza kuona tofauti ya hii safari. Gari lilikuwa linatembea taratibu sana. Hakukuwa na namna wala cha kusubili madereva wawili waliokuwa mbele walionekana kufanya jitihada kubwa ili safari isilale.
"Tunaweza kuingia Kasulu saa kumi na moja kwa huu mwendo!", abiria mmoja nyuma yangu aliongea na mwenzake jirani.
"Leo eeeh kazi ipo na barabara yetu hii! Alijibu.
Mmmmh ni hatari, tuombe Mungu sana". Aliongeza tena.
Wakati haya maongezi yanaendelea basi lilisimama na safari hii kila mtu alihamaki na kuduwaa. Gari kubwa la mizigo lililokuwa linatoka upande wa Kasulu lilikuwa limekwama kwenye tope kutokana na uzito wa mzigo, katika jitihada za kulitoa likawa limefunga barabara kabisa na kufanya magari mengine yasiweze kupita. Ikatubidi tushuke abiria wote ndani ya basi, wakuchimba sawa wakaenda wengine tukatulia tu kuangalia jitihada za matingo na madereva katika kulitoa lile 'semi'. Nikawa mpole.

"Hizi safari mbona nina balaa nazo, tuombe Mungu hilo gari lililozuia njia walitoe la sivyo sijui labda tutafutiwe utaratibu mwingine wa kwenda!" Alisema mwanamke mmoja ambae tulikuwa tumesimama naye kushang'aa jeki zilivyokuwa zinashindana kulipandisha gari kwa juu ili walau waweze kulipunguza lile tope na kuweka mawe k**a moja ya mbinu ya kulikwamua mule topeni. Kwa muda mfupi tu msururu wa magari ulikuwa umepanga foleni kungoja fadhila la hili semi ambalo limekuwa kikwazo na kwa jinsi njia ilivyokuwa hakuna hata dereva aliyekuwa na ujasiri wa kutanua pembeni maana palikuwa pamebana, halafu upande wa juu ulikuwa na miti mikubwa uliofanya pasiwe na uwezekano wa kuipenya hata kidogo na kwa chini palionekana tepetepe sana kiasi ambacho hawakudhubutu kupenyeza nagari yao. Wote wakawa wapole, si magari yaliyokuwa yametokea upande wa Kasulu wala Kidondo yote yalikaa kwenye foleni.

"Kwa wale wasafiri tuliokuja nao kuna gari linakuja lakini wataondoka wale tu ambao hawana mizigo yao kwenye buti", konda wa basi letu alituambia. Kuangalia saa "duuuh" kumi na mbili kasorobo, eeeehee kazi ipo leo! Tuliokuwa na vibegi tu tukavichukua kusubilia hilo linalokuja ambalo nalo pia hatukuambiwa linatokea wapi, Kigoma mjini au Kasulu. Tukalisubiri basi mkombozi wa hatma ya safari yetu.

Jitihada nyingi zilifanyika kusaidia walau abiria wa mabasi waweze kuondoka kutoka maeneo yake ambayo yalikuwa ni ya porini. Gari la polisi punde likafika likiwa na polisi karibu kumi na trafiki wanne wakaangaliaangalia hali ilivyo na kuongea na madereva kwa kirefu kisha wakatutia moyo na kututaka tusiwe na wasiwasi wowote. Kila abiria alikuwa na woga mwingi kwani muda ulikuwa umeenda sana. Kwa mara ya kwanza harufu ya kulala nikiwa safarini ikanukia. Kwa wanaofahamu maeneo yale niliwasikia wanasema "tulikuwa tunakaribia Makere". Hali ya mawingu ilianza tena kuashiria dalili zote za mvua kunyesha.
Nikachukua simu yangu walau nifanye mawasiliano "network searching" nikachoka, nikachukua biskuti kwenye begi nikaanza kula huku tukikodolea macho basi tuliloambiwa linakuja kutufaulisha.
Muda ulisogea, saa zilisonga basi tuliloambiwa linakuja halijafika, tuliweweka na kujawa na hofu za kulala pale!.

Itaendelea.

Comment & share
Zaidi
Email : [email protected]
Whatapp: 0757536278.

06/05/2017

SAFARI ISIYOSAHAULIKA.

Sehemu ya II.
-------------------------------------------------------------------

Baada ya kusimama kwa muda safari ya Mathias iliendelea ndani ya basi alilokuwa amepanda, basi la kampuni iliyokuwa imejizolea kila aina ya sifa kwa abiria apitaye njia hii. Basi la kampuni ya Adventure ndimo Mathias alikuwa amepanda.

Sasa endelea!!

*****
"Fungeni vioo" ilikuwa ni sauti ya abiria mmoja aliyekuwa amekaa siti ya nyuma yangu upande wa dirishani. Hewa nzito na yenye mchanganyiko wa vumbi ilianza kutukwaza mle ndani kiasi ambacho kilimfanya mama aliyekuwa amekaa pembeni yangu aanze kutapika!
"Jamani dereva utatuua" alianza kulalama.
"Pole mama! Tatizo hili na wee unalo?" Abiria aliyekuwa naye siti hiyo alimsemesha.
"Baba, yaani safari imezidi sijawahi kuona tangu nianze kusafiri maisha yangu yote! Huwa sina hili tatizo hata mimi nashangaa!"
"Ulishawahi kupita hii njia?"__
"Hapana! Hii ndio mara ya kwanza kuja huku". Yule Mama alijibu.
"Kaza moyo bado tuna safari". Alisema.

Niliyasikiliza yale maongezi wala sikushangaa kwani njia hii sikuwa mgeni hata kidogo kwani nilishawahi kupita mara kadhaa. Tofauti ya safari hii nilikuwa sijawahi kusafiri masika ndio shaka niliyokuwa nayo na ambayo taratibu ilianza kujenga hofu kichwani mwangu!
"Kigoma we pasikie tu k**a unakuja huku lazima uandae safari kwelikweli, kiroho na kimwili! Nilivyokuangalia tu unaingia na kukaa hapa karibu yangu nikajisemea moyoni, Huku huwa hakuna ubishoo". Huku utalowa vumbi tena na hivi ni masika lazima utapakae tope alafu nguo yenyewe umevaa nyeupe nakuambia hauta ivaa tena maana haita takata hata uifuaje na kwa sabuni gani!

"Tutasimama Kakonko dakika kumi na tano tu hivyo k**a utakunywa chai ufanye haraka...", Sauti ya Konda ilisikika akitoa maelekezo.
Nikamuuliza jirani tangu tulikuwa nae ambaye muda wote alikuwa bize na simu yake akichati na kusikiliza muziki kwa earphones. "Kumbe tusiposimama simama sana tutafika mapema!"
"Watakuwa wamenisaidia sana maana ninaweza kuwahi boti la jioni". Alisema.
"La kwenda wapi? Niliuliza.
"Kagunga". Alijibu.
"Oooooh sawa! Tuombe Mungu bado tuna safari ndefu sana!" Nilisema.
Majira ya saa nne hivi tukiwa tumeongozana na magari mengine mawili tukafika Kakonko basi letu lilisimama na abiria tukashuka wengine tukaenda kunywa chai wengine wakabaki jirani ya basi ili kupunga na kubadilisha hewa.

Honi kali ilipigwa na kutufanya tush*tuke na baadhi yetu tuache chai na kubeba chapati na mandazi na kuingia nayo kwenye gari. Walau muda ule tuliopumzika walau kila abiria alionekana kuwa na hamu tena ya safari. Nilisogea na nikaa kwenye siti yangu muda huu gari lilikuwa limeanza kuondoka tayari.
"Mmphhhh" nilipumua pumzi ndefu kuashiria tunaanza tena safari.
Muda huu hali ya hewa ilikuwa imeanza kuwa nzito hali hii hakuna aliyeshangaa k**a anauzoefu na hali ya masika ya mkoa wa Kigoma, masika yake huwa na mvua nyingi. Gari lilianza kuchanganya mwendo, abiria walikumbushwa kufunga vioo na vumbi zito lililokuwa limeanza kujaa ndani kwa mara nyingine.
Safari ikaendelea abiria wote tukaa kimya ilisikika sauti ya dereva na konda wake tu waliokuwa wanazungumza kuhusu mzigo wa madumu walioupakia kule Nyakanazi kuwa ulikuwa unatakiwa ushushiwe Kahabwa.

Sauti zilisikika zikiimba nyimbo huku wakipiga kelele zilizokuwa k**a zinatia hamasa...."tumefika Kanembwa, hao ni JKT wanakimbia mchakamchaka maana manyimbo yao yanafurahishaga sana", yule Baba aliyekuwa pembeni alisema. Tukaanza kuzisikia kwa karibu, ghafla basi letu likasimama.
Kwa kuwa nilikuwa siti ya dirishani, nilifungua dirisha na kuangalia mbele ili nione ni kitu gani kimejili kilichosababisha tusimame kambini pale. Hakukuwa na chochote zaidi waliingia wanajeshi wawili na basi lilianza tena safari. Wakati huo karibu kila abiria aliingiwa na hofu kwa kusimamishwa kwa gari letu lakini hapakuwa na sababu yoyote.
"Nilidhani watatukagua vitambulisho", ilisikika sauti ya abiria mmoja kwa mbele ya nilipokuwa nimekaa.
"Msiwe na hofu maeneo haya sasa hivi yana usalama wa kutosha, sisi tunaenda Burombola kidogo", alisema mwanajeshi mmoja kati ya wale waliopandia pale kambini.
Wakati huu manyunyu yalikuwa yameanza taratibu na kupoza vumbi zito lililokuwa likitusumbua mle ndani wakati huo.

"Hatutapita stendi abiria wa Kibondo wajiandae..." Konda alitangaza. Abiria waliokuwa wanatakiwa kushukia hapo walianza kujinyoosha na kuonyesha tabasamu la kufika salama.
"Halloo! Tumefika Kibondo muda huu", niliongea na mama.
Oooh! Sawa mtafika mapema sana. Mungu awatangulie katika safari", mama aliongeza.
"Ok! Sawa mama!"
Waliokuwa wanashukia pale wakashuka na safari ikaendelea. Gari lilichanganya, muda ukazidi kwenda vimanyunyu vikakata hali ya anga ikawa shwari kabisa mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea miongoni mwa abiria ndani ya gari, kwa ufupi binafsi nilikuwa sawa!.

Tukapita vijiji vingi tu, hatukusimama simama ila mabadiliko ya wingu zito lililosababisha giza lililomfanya dereva kuwasha taa, lilitutia hofu ghafla.
"Hizi mvua za Kigoma nazo zisizoisha hadi kero". Alisema mzee mmoja ambae muda huo alikuwa anatafuna karanga alizokuwa nazo kwenye mfuko.
Wingu likazidi, likazidi likafunika anga lote! Dereva akaanza kutembea taratibu lakini hali ya hewa ikawa mbaya sana.
"Tunasimama hapo mbele hali ya anga ni mbaya" dereva alimwambia konda.
Kila mtu alianza kusali na kuomba Mungu kimoyomoyo maana hakuna aliyekuwa anaona nje, giza likawa giza. Tulisimama Nyakitonto kwa usalama zaidi, hali ya anga haikuwa inaruhusu kabisa. Mvua kubwa ikaanguka, mvua ya mawe ikanyesha!, ikanyesha! Ilikuwa kubwa ajabu! Lakini kadiri ilivyokuwa inanyesha hali ya hewa nayo ikaanza kuwa angavu. Pakawa shwari baada ya saa mbili hivi, dereva na konda wakajiridhisha tukaanza safari tena. Huu ndio ikawa mwanzo wa safari yangu nisiyoweza kuisahau!

Itaendelea...

Kwa ushauri na maoni.
Tuma message au comment.
Email : [email protected]
Whatapp: 0757536278.

06/05/2017

SAFARI ISIYOSAHAULIKA.

Sehemu ya I
-----------------------------------------------------------------

Mathias! Mathias!...Amka pamepambazuka! Sauti ya mama iliniamrisha niamke ili nijiandae kuelekea kituo cha mabasi.
"Mmmmmphh!! Kwani saa ngapi?", Niliuliza huku nikiweweseka kitandani kwa wingi wa usingizi.
"Haufanyi haraka wee endekeza kulala sasa ilishakuwa saa kumi na mbili na nusu!" Alisema.
"Sawa nitawahi tu bila shaka hapo kwa kwenda dakika tano tu!" Nilimtoa hofu mama.
Mara zote nikiwa na safari ambayo ilinilazimu kuamka mapema mama yangu alikuwa makini sana kunikumbusha kwa kuniamsha kwa aliyajua mazoea yangu ya kulala 'fofofo' na kujishtua wakiwa wanakunywa chai.

Nilitoka nje nikapiga 'pushup' mbili tatu kisha nikaelekea bafuni kuoga. Kwakuwa nilikuwa nimekwisha andaa kila kitu kwa safari ya leo, haikunichukua muda mwingi kujiandaa. Nikachukua simu yangu nikampigia Pasco. "Haloo! Vipi? Pamekucha mzee baba njoo tusepe!"
"Okay, makini natimba soon!"
Huyu ndiye mtu ambaye safari zangu zote nilikuwa namtumia kunifikisha stendi. Ni jama'ngu wa kitaa mwendesha bodaboda kwa muda sasa tangu kipindi sisi tunaharakati za kusoma.

Nilichukua begi langu la mgongoni na kumwita mama, "Mama mi naondoka!"
"Sawa, safari njema! Ukifika usisahau tulivyoongea!" Alisisitiza.
Nikatoka tayari kwa kuanza zangu safari kwani Pasco alikuwa ameshafika.
"Niaje boy, naona kibaharia zaidi!" Alinisabahi. "Fresh kaka twenzetu time imesonga".

Ulikuwa ni mwendo wa karibu dakika sita tu kutoka nyumbani tukawa tumeshawasili stendi ya mabasi mjini Kahama."Poa mwana, safari njema!"
Asante! Nikaelekea tayari kupanda gari.
"Wapi? Wapi? Tabora, Dar, Arusha" alinidaka mpiga debe mmoja", "Achana naye, janja wapi Nzega au Mwanza?" Ukifika stendi hali haiepukiki nilishazoea.
"KG", nilijibu, "Twenzetu! Tiketi unayo? "Nilikata jana Adventure!"
Lile pale linakaribia kuondoka.
Nikatafuta siti yangu nikakaa.
Safari ilianza nikiwa na "mood" ya kutosha kabisa kwani ilikuwa nimeshazoea safari za Masada narefu kwa kiasi cha Mimi kutokuwa na shaka ya safari hii.

Safari ilianza kwa pishanapishana ya mabasi michezo ambayo kwa madereva ni kawaida, punde tukafika Nyakanazi. Akili yangu sasa ndio ikaanza kuwaza sasa kuwa nipo safarini. Gari letu nikakata kona kuashiria uelekeo wa safari ya Kigoma inaanza. Tuliacha barabara ya rami kidogo alafu kukasimama kwa kupakiwa mzigo wa madumu ambayo yaliashiria kuwa wanayapeleka Kigoma ili wawekee mafuta ya mawese kwa muonekano wake. Muda huo wanapakia ndipo tulipopata wasaa wa kununua chochote k**a kifungua kinywa

Ilikuwa masika msimu wa mvua kwa wazoevu walianza kusikika wakisena "Hili tope tutalipona kweli". Kwa kuwa nami nilikuwa sio mgeni kwenye safari njia hii niliwaza kimoyomoyo "kazi ipo"
"Abiria fungeni mikanda" alisikika sauti ya trafiki aliyekuwa amemaliza kuongea na makondakta wa gari. Safari ilianza ndipo kila abiria alinza kutoa mnong'ono "Huu mziki tutauweza kweli?"

Itaendelea...

Usisahau ku-like na ku-share!!

Mawasiliano & Ushauri.
Email: [email protected]
Whatapp: 0757536278.

Address

Chanika, Ilala
Dar Es Salaam

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Ujamaa Online posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share