26/05/2026
Mamilioni ya waumini wa dini ya Kiislamu kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekusanyika leo Jumanne katika viwanja vya Arafat nchini Saudi Arabia, katika kilele cha ibada takatifu ya Hajj.
Mahujaji hao wamefanya ibada muhimu ya kusimama katika Mlima Arafat, hatua inayochukuliwa kuwa nguzo kuu ya Hija, huku maelfu wakitumia muda huo kuswali, kufanya dua na kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha wa dhambi zao.
Licha ya hali ya taharuki na vita vinavyoendelea katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati, mamlaka za Saudi Arabia zimesema idadi ya mahujaji kutoka mataifa ya nje imeongezeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2025.
Maelfu ya mahujaji wameonekana wakimiminika katika eneo la Arafat tangu alfajiri, huku serikali ya Saudi Arabia ikiendelea kuimarisha huduma za usalama, afya na usafiri ili kuhakikisha ibada hiyo inafanyika kwa utulivu na usalama.
Ibada ya Hajj ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu na hukutanisha Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani kila mwaka katika miji mitakatifu ya Makka na maeneo yanayozunguka.